IQNA

Jinai za Israel

 Askari vamizi wa Israel waunajisi Msikiti wa Jenin na kuua Wapalestina 12

18:52 - December 15, 2023
Habari ID: 3478037
IQNA – Askari wa jeshi vamizi la Israel wameuhujumu na kuunajisi msikiti mmoja huko Jenin wakati wa shambulio lililosababisha vifo vya Wapalestina 12 siku ya Alhamisi.

Video zilizosambazwa na vyombo vya habari vya utawala haramu wa Israel na maafisa wa utawala huo, akiwemo waziri wa mambo ya ndani mwenye itikadi kali Itamar Ben-Gvir, zinaonyesha wanajeshi vamizi wa Israel wakiimba nyimbo za Kiyahudi kupitia kipaza sauti cha msikiti wa Jenin katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Video moja, iliyotolewa na gazeti Haaretz, inaonekana inaonyesha askari hao wakiimba wimbo wa Hanukkah wenye anuani  ya Tumekuja Kuondoa Giza.

Nyingine inaonyesha mwanajeshi wa Israel akiwa amekaa kwenye sakafu ya msikiti akizungumza kwenye kipaza sauti cha adhana akisema: "Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema. Huyu hapa msemaji wa Jeshi la Israel," anasema, katika dhihaka dhahiri ya adhana.

Wanajeshi wanaonekana wakiingia msikitini huku wakiwa wamevaa viatu, kitendo ambacho ni kuvunjia heshima eneo hilo takatifu la Waislamu la ibada.

Nabil Abu Rudeineh, msemaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, amelaani kitendo hicho na kusema ni kukitaja kuwa cha cha "aibu", akionya dhidi ya kuliingiza eneo hilo kwenye vita vya kidini.

Msemaji huyo rasmi wa Ofisi ya Rais ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa hususan Marekani kuweka mashinikizo kwa Israel kuacha ukiukaji wake dhidi ya watu wa Palestina, mali zao na maeneo yao matakatifu, akisisitiza kuwa mashambulizi hayo yanakuja ikiwa ni mwendelezo wa mashambulizi dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem).

Tangu Oktoba 7, utawala katili wa Israel umewauwa karibu Wapalestina 19,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wakati wa uvamizi unaoendelea wa kijeshi kwenye Ukanda wa Gaza uliozingirwa. Aidha vikosi vya Israel vimewaua Wapalestina wasiopungua 287 katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu katika kipindi hicho.

Habari zinazohusiana
captcha